Thursday, March 19, 2009

WAKILI ALIA MAHAKAMANI: Si Usanii huu kweli?

Na Mary Edward, Dodoma

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Wakili aliyekuwa akimtetea Deus Mallya aliyeshitakiwa kwa kusababisha ajali iliyomuua mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe, Godfrey Wasonga, ameangua kilio mahakamani baada ya mteja wake kupatikana na makosa na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. 

Mallya amepatikana na hatia ya makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili, moja la kuendesha gari kwa mwendo wa hatari na pili kuendesha gari bila ya kuwa na leseni na kusababisha ajali iliyokatisha uhai wa Wangwe. 

Akisoma mashitaka hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Thomas Simba, alisema ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa huyo umeonyesha ni kweli alikuwa akiendesha gari siku hiyo na bila leseni. 

Alisema pamoja na mshitakiwa kujitetea kuwa hakuwa anaendesha gari na hajui kuendesha gari, ushahidi wa shahidi namba 3 ambaye ni fundi magari na namba 9 pamoja na ushahidi wa namba moja na mbili ambao ni watoto wa marehemu umeonyesha Mallya ndiye alikuwa akiendesha gari. 

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Simba ambaye aliisoma hukumu hiyo kwa muda wa saa mbili alisema kwa mujibu wa sheria namba 63 kifungu kidogo cha pili sura ya 168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mtuhumiwa anayepatikana na makosa hayo anatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu au zaidi. 

Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Simba alimpa nafasi Wakili wa Mallya, Wasonga kutoa utetezi wa mwisho kwa mteja wake ambapo katika hali isiyokuwa ya kawaida alianza kulia mahakamani na kushindwa kufanya hivyo. 

Baada ya kama dakika tano, ndipo Wasonga aliiomba mahakama itoe faini kwa mteja wake kwa kuwa kosa hilo ni la kwanza na baadaye alikwenda kwa mteja wake na kumnong`oneza maneno ya kusema wakati wa kujitetea. 

Hata hivyo, katika hali inayoonyesha kuwa Mallya alichanganyikiwa baada ya kutiwa hatiani alishindwa kujitetea na kuanza kutoa maelezo ya awali aliyoyatoa wakati wa utetezi wakati kesi hiyo ikisikilizwa, hali ambavyo ilimfanya wakili wake asimame na kwenda kumfundisha namna ya kujitetea. 

Ndipo katika utetezi wake, Mallya aliiomba mahakama impe adhabu ndogo kwa kuwa ana wazazi na mdogo wake wanaomtegemea na pia aliongeza kuwa ana watoto yatima anaowasomesha na wafanyakazi wanaomtegemea katika ofisi yake. 

Ndugu na jamaa za Mallya waliofika mahakamani hapo, walionekana kuchanganyikiwa huku wengine wakiangua kilio mara baada ya hukumu hiyo. 

Mallya alifika mahakamani hapo jana saa 2:00 kamili asubuhi akiwa na ndugu yake mmoja kwenye gari ndogo ambapo wakati wote alionekana mchangamfu na mtulivu. 

Baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo kushuhudia hukumu hiyo alikuwa akizungumza nao na kuonyesha kuwa hana wasiwasi wa hukumu hiyo, lakini alipoingia tu mahakamani alibadilika gafla kuwa na wasiwasi na wakati wote alikuwa akishika tama kama mtu aliyekuwa akifikiria jambo. 

Mallya alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti Mosi mwaka jana baada ya kupona majeraha madogo aliyokuwa ameyapata katika ajali na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma . 

Ajali hiyo ilitokea Julai 28 mwaka jana majira ya saa 2:00 usiku wakati Mallya na Wangwe wakiwa njiani kuelekea jijini Dar es Salaam huku Mallya akiendesha gari dogo aina ya Corolla lenye namba za usajili T 865AMR mali ya marehemu Wangwe. 

Mallya alidaiwa kuendesha gari kwa mwendo kasi ambapo tairi la mbele upande wa kulia lilipasuka na gari kuhama barabarani na kisha kupinduka. 

Kesi hiyo ilikuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakihudhuria mahakamani kusikiliza, kutokana na ufinyu wa chumba cha mahakama ambamo kesi hiyo ilipokuwa ikiendeshwa iliwalazimu wananchi wengine kukaa nje ya chumba cha mahakama wakati kesi ikiendelea jana. 

Katika kesi hiyo, jumla ya mashahidi 10 upande wa mashitaka walitoa ushahidi wao wakiwemo watoto wawili wa Marehemu Wangwe ambapo ni Wangwe na Abinego Bukuru, hata hivyo, wakati hukumu hiyo ikitolewa, hawakuwepo mahakamani. 

  • SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment