| Polisi wadaiwa kuua raia Dar |
Na Geofrey Nyang'oro POLISI wa kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu wanadaiwa kumshambulia kwa risasi na kumuua dereva mmoja wa teksi ambaye ni mkazi wa Kimara Stop Over licha ya kijana huyo kutii amri ya kusimamisha gari. Tukio hilo lilitokea Machi 24 Mtaa wa Stop Over Kiwanjani baada ya dereva huyo, Lazaro Mwapi, mwenye umri kati ya miaka 23 na 24, kusimamishwa na askari waliokuwa doria wakati akirudi kituoni kwake maeneo ya Kimara Suca. Mauaji ya kijana huyo yanadaiwa kufanywa siku na wakati ambao eneo hilo lilikuwa limevamiwa na majambazi wenye silaha ambao walipora maduka mawili. Waliovamiwa kwenye tukio la siku hiyo ni pamoja na Damas Mtenga, ambaye alijeruhiwa kwa panga na kuporwa vitu mbalimbali pamoja na fedha na Ibrahim Paulo aliyepigwa na kuporwa Sh700,000 pamoja na simu ya mkononi. Kwa mujibu wa madereva teksi wa kituo hicho, siku ya tukio dereva huyo aliondoka na abiria anayefahamika kwa jina moja la Mtenga majira ya saa 3:45 usiku na kumpeleka nyumbani kwake Mtaa wa Mpangala. Nuru Omari alisema baada ya kumfikisha abiria huyo alikuwa akirudi kwa kupitia njia ya Kwa Mpangala na kabla hajafika mbali, alikutana na mama mmoja aliyemshauri abadilishe njia kwa kuwa njia aliyokuwa akielekea kulitokea tukio la ujambazi. Alisema baada ya ushauri huo, Mwapi alibadilisha njia na kupita barabara ya Stop Over. Lakini akiwa katika barabara hiyo Mtaa wa Stop Over Uwanjani, dereva huyo alikutana na watu waliokuwa wamevalia nguo za kiraia wakiwa na silaha na kumuamuru asimamishe gari, jambo ambalo kijana huyo alitii. Baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini walisema walisikia sauti ya watu wakizungumza kwa ukali katika neo lililo karibu na makazi ya watu wakisema "simamisha gari sisi ni askari". Mashuhuda hao walisema maneno ya dereva huyo hawakuweza kuyasikia vizuri kwa kuwa gari lilikuwa limefungwa vioo na hivyo kusikia zaidi askari waliomtaka kijana huyo kushusha vioo na kuwasha taa za ndani mambo ambayo inadaiwa dereva teksi huyo hakuyatekeleza. Shuhuda huyo alilieleza Mwananchi kuwa majadiliano hayo yalichukua muda mrefu kiasi, kabla hajasikia mlio mkubwa ulioonyesha kuvunjwa kwa vioo vya gari hilo. Alisema mara baada ya mlio huo alisikia mlio wa bunduki ukilia haraka haraka mara tatu kisha watu hao walisikika wakiwasiliana kwa njia ya simu na wenzao. "Nilisikia ta...ta...ta.... baada ya hapo wakawa wanafanya mawasiliano wenyewe kwa wenyewe," alisema shuhuda mwingine. Alisema baadaye lilifika gari la polisi katika eneo hilo na kupakia mwili wa mtu huyo ambaye shuhuda huyo hakujua kama alikuwa amekufa au la na kuondoka nao huku gari alilokuwa akiendesha lilichukuliwa na askari hao. Mwenyekiti wa chama cha madereva wa teksi kituo cha Kimara Suca, Zuberi Hussein alilieleza gazeti hili kuwa alipata taarifa za kifo cha dereva huyo juzi mchana baada ya dereva mwenzao kuwataarifu kuwa aliliona gari la Lazaro kituo cha polisi Mbezi likiwa limeegeshwa. Alisema taarifa hizo ziliwashitua ndipo madereva wote walipokwenda kituoni hapo na kuelezwa kuwa mwenzao alikutwa kwenye eneo la tukio la ujambazi. Madereva hao walisema wakati wote wakifanya juhudi hizo hawakujulishwa wapi mwili wa marehemu ulikuwa umepelekwa. "Kwa muda wote sisi hatukujulishwa mahali ambapo mwili wa marehemu huyo ulikuwa umepelekwa licha ya juhudi zetu za kutaka kumuona mwenzetu," alisema Hussein. Naye Obeid Suleyman aliyejitambulisha kuwa ndiye aliyekuwa akiishi na dereva huyo aliyeuawa kwa muda wote hadi hapo alipoanza kujitegemea mwenyewe, alisema alipatiwa taarifa za kifo cha kijana huyo juzi mchana. Alisema alishtushwa na habari hizo na ndipo alipokwenda polisi na kuelezwa kuwa alikutwa kwenye eneo la tukio akijihusisha na uhalifu. Alisema polisi kituoni hapo walikataa kuchukua maelezo yake ya namna anavyomfahamu marehemu kwa madai kuwa muda huo walikuwa wanamtaka ndugu yake wa karibu anayeishi naye kwa wakati huu. Jirani wa kijana huyo walionekana kuwa na huzuni na mashaka huku wakililaumu Jeshi la Polisi kwa kuua bila ya kufanya uchunguzi wa kina. Walisema kwa kawaida Lazaro alikuwa mtu wa watu ambaye hata siku moja wasingefikiri kama angeuawa kinyama namna hiyo. Wakizungumzia tukio la ujambazi lililotokea siku ya tukio, baadhi ya watu walioathirika walieleza kushangazwa na taarifa za polisi kumuhusisha dereva huyo na ujambazi. Naye Damasi Mtenga ambaye alivamiwa na majambazi na kuporwa vitu mbalimbali pamoja na kujeruhiwa kwa panga mkononi, alisema kwa mazingira ya tukio lilivyokuwa ni dhahiri kuwa dereva huyo alionewa. Alisema kundi la majambazi lilifika dukani kwake majira ya saa 4:00 usiku wakiwa na silaha za kila aina na kwamba, hali hiyo inamfanya aamini kuwa aliyeuawa siye kwa kuwa kwenye gari alikuwa peke yake. Akisimulia namna majambazi hao walivyofanikisha ujambazi wao, alisema watu wasiofahamika walifika dukani kwake na kumtaka awauzie vocha za simu ambazo yeye hakuwa nazo. Alisema baada ya kuwajibu kuwa hana vocha hizo wateja hao ambao walikuwa hawaeleweki walinunua soda na kukaa kwenye baraza la duka lake kila mtu peke yake. Hali hiyo ya wateja wawili kukaa kila mtu peke yake kama hawajuani ilimpa shaka ndipo alipoanza kufanya uchunguzi ili kugundua walikuwa na nia gani. Alisema alipotoka mara ya pili huku akiwaangalia kwa makini alibaini mmoja wao alikuwa amevaa bunduki aina ya SMG mgongoni, lakini ilionekana kama imevunjwa kitako. Jambo hilo lilimfanya ashituke na kufunga duka kwa nje kisha naye kukaa hapo hapo akiwa na wateja wake wengine pamoja na majambazi hayo. Alisema ghafla jambazi moja lilimtaka amuongezee kinywaji na alipoondoka na kuanza kutafuta njia ya kukimbilia, alitokea jambazi mwingine aliyekuwa mbali na eneo hilo na kumnyooshea bunduki huku akimtaka atulie palepale alipokuwapo. Alisema aliitikia wito huo na kuamriwa kufungua duka kuwaonyesha fedha zote zilizokuwa ndani na kuwataka wachukue kila kitu walichoweza ili mradi wasimdhuru. Alisema majambazi hayo yalichukua fedha taslimu Sh540,000 alizokuwa nazo pamoja na mauzo ya siku hiyo yote. Pia alisema majambazi hayo yaliyokuwa katika kundi yaliwapora wateja waliokuwa katika eneo la duka hilo vitu mbalimbali pamoja na fedha. Naye Amina Manzi alilieleza gazeti hili kuwa baada ya kukamilisha kazi hiyo, majambazi hao walipita karibu na nyumba yao na kumvamia mumewe na kumpora fedha taslimu Sh 700,000 na simu ya mkononi aina ya Nokia. Manzi alisema mume wake alikuwa amerudi kutoka kazini na alipofika aliamua kutoka nje ili kushuhudia kilichokuwa kikitokea baada ya kusikia mlio wa bunduki. Alisema licha ya kupora kiasi hicho pia majambazi hayo yaliendelea kushauriana kuwa wamuue au la ndipo moja liliposema hapa tunapitia wapi na kuondoka zao. Akizungumzia kifo cha dereva teksi huyo alisema kimemsikitisha sana kwa kuwa aliyeuawa ni mmoja wa wapangaji wenzake. Alisema hata siku ya tukio alikutana naye majira ya saa moja usiku akiwa anakula chakula katika eno lake la kazi na kuzungumza naye, lakini alishangaa kuona kijana huyo hakurejea nyumbani kama ilivyokuwa kawaida yake na alipompigia simu, haikupokelewa. Mwanachi ilishuhudia gari lililokuwa likiendeshwa na kijana huyo likiwa limeegeshwa kwenye kituo cha Polisi cha Mbezi. Kioo cha mbele cha upande wa kushoto kimevunjika na ndani ya gari hilo kuna alama za damu. Wakazi wa Kimara walielezea kusikitishwa na kitendo hicho na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo. Mwananchi ilipomtafuta kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam kuzungumzia suala hilo alisema bado halijafika kwake na kwamba msemaji wa hilo kwa sasa ni kamanda wa mkoa wa Kinondoni. Kamanda wa mkoa wa Kinondoni, Mark Kalunguyeye alitafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi kuzungumzia suala hilo, lakini hakupatikana. |
Friday, March 27, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment