Friday, April 10, 2009

KIKAO CHA BARAZA LA JUMUIYA YA WATANZANIA TAMIL NADU





Mnamo tarehe 4 April 2009. Viongozi wa jumuiya ya watanzania Tamil Nadu wakiwemo viongozi wa kamati tendaji na wawakilishi wa matawi ya jumuiya kutoka miji husika walikutana mjini Tirruchchirapalli (Trichy) kwa ajili ya kikao cha kwanza cha ngazi ya baraza kama ilivyoainishwa kwenye katiba ya jumuiya.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa kamati tendaji pamoja na viongozi wa miji ya Trichy (wenyeji), Madurai na Chennai. Kikao hiko pia kilihudhuriwa na waalikwa kutoka miji ya Ooty na Erode kwa ajili ya kuja kujifunza na kubadilishana mawazo na uzoefu.

Miongoni mwa mambo yaliyaojadiliwa ni vipaumbele katika utendaji wa jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2009, namna ya kuwahamasisha watanzania wa miji mingine kujiunga na jumuiya na taratibu za kiutendaji za baraza la jumuiya.

Akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Tamil Nadu Ndg. Deus Valentine Rweyemamu aliainisha kuwa wakati wa kuandaa Kongamano la watanzania Tamil Nadu kipaumbele kilikuwa ni kuwakusanya watanzania waliopo Tamil Nadu. "Wakati wa kongamano tulijikita kujadili ni namna gani tutautunza na pale inapowezekana kuupanua mkusanyiko wetu, na ndipo wazo la kuunda jumuiya lilipoanzia kwahiyo tukaridhia na kupitisha katiba ili tuwe na chombo rasmi cha kutukusanya sisi kama Watanzania tunaoishi katika jimbo hili la Tamil Nadu."

Wajumbe walikubaliana kimsingi kwamba Jumuiya hii si chombo cha kisiasa ila ni utaratibu wa kurahisisha mahusiano ya kijamii kwa watanzania waliopo Tamil Nadu. Jumuiya itakuwa imefanikisha malengo yake kama mwisho wa siku itapelekea watanzania wa Tamil Nadu kujumuika zaidi, kufahamiana zaidi na kushirikiana zaidi.

Kulingana na Katiba ya jumuiya ya Watanzania Tamil Nadu kama ilivopitishwa Tarehe 26 Disemba 2009 Baraza la Jumuiya ni chombo cha maamuzi kinachoundwa na kamati tendaji na wawakilishi wa kila tawi. Baraza hili husimamia utendaji wa Kamati tendaji na ni chombo kinachotumika kuyashirikisha matawi yote katika kufanya maamuzi na hivyo kuwa na dau sawa (equal stake) katika uendeshaji wa jumuiya. Baraza hili kulingana na Kaitba hukutana kila baada ya miezi mitatu.

Tunatarajia kuwashirikisha habari zaidi punde tutakapopata miniti za kikao hicho kutoka kwa ofisi ya Katibu mkuu pamoja na tamko la baraza lilitokana na kikao hicho.

Tunawashukuru sana washiriki wa kikao kwa moyo wao wa dhati wa kujitolea. Wajumbe walikuwa tayari kujighramia kuhudhuria kikao hichi kwa moyo mkunjufu wakielewa wazi kuwa Jumuiya bado ni changa na haina uwezo wa kujiendesha ipasavyo kwa sasa. Tunawashukuru sana wenyeji wetu Trichy kwa kujitolea muda wao na kwa kuwa tayari kuchangia sehemu ya gharama za kikao.

Tunawashukuru vile vile dada zetu wa Madurai kwa kukubali kuwa wenyeji wa kikao kijacho cha baraza.

Kwa mawasiliano zaidi kuhusu kikao hichi pamoja na Ajenda zake wasiliana na Idara ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano kupitia watanzania.tamilnadu@yahoo.com.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu awabariki nyote.

Aluta Continua!!!

Imetolewa  na Idara ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano.
Jumuiya ya Watanzania Tamil Nadu.

No comments:

Post a Comment